MAANA
YA WAHUSIKA NA UHUSIKA KATIKA KAZI ZA FASIHI ANDISHI.
Wahusika
ni watendaji au viumbe katika kazi ya fasihi. Wao ndio nguzo kuu wa dhamira na
maudhui kwa sababu ni kupitia kwao ndipo huweza kujitokeza katika kazi ya fasihi.
Wahusika wanaweza kuwa
wanyama, binadamu wenyewe ama vinyago ambavyo vinafanana kwa kiasi kikubwa na
binadamu katika maisha ya kawaida. Hata hivyo si lazima wadhibitiwe na kanuni
zote za binadamu halisi.
Ni muhimu kuwajua
wahusika pamoja na umuhimu wao kwa sababu hii itamwezesha mhakiki kuichambua na
kuielewa kazi ya fasihi vyema hasa tukizingatia maudhui na dhamira ya
mwandishi.
Wahusika hutumiwa
kuwasilisha hali halisi ya maisha ya binadamu katika jamii fulani. Mhakiki
anapaswa kujua majina yao, maneno wanayoyasema, maelezo ya mwandishi kuwahusu,
matendo yao, maneno ya wahusika wengine kuwahusu, dhima zao, mitazamo,
kukubalika kwao kifasihi na uchangamano wao na ukamilifu wao kisaikolojia,
kimatendo au kijamii.
Uhusika
ni
ile hali au sehemu inayochangiwa na wahusika katika kazi ya fasihi. Mchango huu
unaweza kuonyeshwa kupitia kwa vitendo vyao, mazungumzo yao, mawazo yao au hata
kwa vitendo na malengo yao.
Wahusika
na uhusika hutumiwa kwa lengo la
kuonyesha ufaafu wa kazi fulani ya fasihi.
Aina
za wahusika.
Kuna wahusika wa aina nyingi:
- Wahusika wakuu.
Hawa husheheni ufanisi wa kazi husika kwa sababu matendo na migogoro yote muhimu inawahusu. Dhamira kuu ya mwandishi hujitokeza kupitia kwao, na msimamo wa mwandishi kuhusu dhamira, matukio na vitushi vya kazi ya fasihi hujibainisha kupitia kwa matendo na maneno yao. Mwingiliano wao na wahusika wengine ndiyo mbinu ya kufafanua dhamira kuu. - Mhusika mkwezwa.
Huyu mhusika ana sifa za kiutendaji. Yeye huinuliwa na kukwezwa na mwandishi. - Mhusika wa kisaikolojia.
Mhusika huyu hukumbana na matatizo mengi ya kijamii na anaibusha hisia za huruma kwa wasomaji. - Mhusika wa kimapinduzi.
Mhusika huyu anaelewa historia, siasa, mazingira na hali ya kiuchumi ya jamii yake. Yuko radhi kujitoa mhanga kubadilisha maisha ya wanyonge. Ana itikadi kali na msimamo thabiti. - Mhusika jumui.
Ni wahusika wengi katika mhusika mmoja. Mhusika huyu huwa na sifa za wahusika wengi. Hupatikana zaidi katika fasihi ya kidhanaaishi. Hutumika kuonyesha fujo katika maisha. - Wahusika wasaidizi.
Hawa hutumiwa ili kumsaidia msomaji kumwelewa vyema mhusika mkuu. Kupitia mwingiliano baina ya mhusika mkuu na mhusika msaidizi, msomaji anapata mwanga zaidi kuhusu hulka ya mhusika mkuu. - Wahusika wajenzi.
Hawa wamewekwa kwa lengo la kukamilisha dhamira na maudhui ya mwandishi. Pia, wanajenga wahusika wasaidizi na wahusika wakuu. Huwakilisha jamii pana, na matendo yao, aghalabu, huonekana kama kwamba ni ya pembezoni japo ni muhimu katika kuulewa muundo wa jamii. - Wahusika duara au miraba minne.
Hawa wahusika wana sifa nyingi ambazo hubadilikabadilika kuwa nzuri au mbaya. Matendo na maisha yao yanaongozwa na hali halisi za maisha. Maisha yao ni mapana, katika tajriba na matukio na huonekana kama binadamu wa kawaida. - Wahusika wa mramba mmoja au bapa.
Hawa huwa na sifa moja tu kama ni wabaya au wazuri. Hubaki vile tangu mwanzo hadi mwisho hata wakati mazingira au mahusiano yabadilikapo. - Wahusika bapa-sugu.
Huwa hawabadiliki na huonyesha msimamo wao kupitia maelezo ya msanii. Ni sugu katika hali zote za maingiliano yao na wengine. - Wahusika bapa-vielelezo.
Hawa huwa hawabadiliki kitabia na hupewa majina ya majazi ambayo yanamwelekeza msomaji na huwa kielelezo cha tabia nzuri au mbaya. Wahusika hawa hutumiwa kama kielelezo cha tabia hiyo. - Mhusika nguli.
Ni mhusika anayeendeleza maadili ya jamii. - Wahusika shinda.
Hawa wako baina ya wahusika duara na bapa. Wana uhai na nguvu zaidi kuliko wahusika bapa. Wanaendelezwa na hawa wahusika wa aina mbili yaani mhusika duara na mhusika bapa.
MAREJELEO
= Njogu,
K. na Chimerra, R. (1999) Ufundishaji wa
Fasishi: Nadharia na mbinu. Nairobi- Jommo Kenyatta Foundation.
= Owen
Mconyango (2006) Mimba ingali mimba na hadithi
nyingine. Focus Publishers
= Syambo,
K. Mazrui (1992) Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi:
East Africa Education Publishers.